Turudishe Ukoloni??

Kuna watu (hasa wazungu) huona matatizo ya kisiasa na kiuchumi ya Afrika kama ushahidi kuwa hatuwezi kujitawala. Watu hawa pia huona kama wakoloni walilikimbia bara letu mapema mno na huenda wangekaa zaidi kidogo. Haya mawazo yamo hata kwenye vichwa vya waafrika. Tatizo ni kuwa hawathubutu kusema kwa kuogopa kuitwa wasaliti na malimbukeni.

Sishangai wala kulaumu wanaofikiri kuwa mwafrika hana akili. Miaka 40 imepita na hatuna cha kuonesha. Mwafrika kamweka mwafrika mwenzake kwenye alama ya kuuliza. Imani imepungua na hata kujiamini nako kumepungua miongoni mwa waafrika. Uhuru umeleta nini kwa waafrika wengi?

Hiki ni kipindi waafrika wakiambiwa kuwa hawana akili kama wazungu, huamini mara moja. Maana wanaona dhahiri kuwa wameshindwa kujitawala na nchi za kizungu (bara Ulaya na Marekani) zinaendelea kuwa tajiri. Afadhali wakati wa ukoloni tulikuwa tunaona kama tunaonewa na huenda ingefika siku moja tungejitawala na kuwa hata zaidi ya wazungu.

Kuna wakati nilisikitika sana mtanzania aliponiuliza tukiwa tumekaa kwenye viti virefu kama muda wa wazungu kurudi umefika. "Kama weusi tumejaribu miaka 40 na hakuna kitu, kwa nini tusiwaachie wanaoweza watawale? Ninamaanisha wazungu!" Jamaa alikuwa hatanii. Pembeni kulikuwa na watu waliomsikia. Walipiga makofi huku wakicheka na mmoja kumjibu kuwa kaongea 'pointi'.

Kwa namna moja au nyingine, wazungu wameanza kurudi kijanjajanja. Wamekuwa wakija kwa njia za 'mashirika ya misaada', mabenki, na 'ma-TX' walioalikwa na serikali kuja kusaidia kutoa ushauri wa kiufundi. Ma-TX wengine hawatoi ushauri tu, wameanza kupewa uongozi wa moja kwa moja wa nchi husika. Mifano ni Sierra Leone na Msumbiji. Mkuu wa polisi wa Sierra Leone ni mzungu wa Uingereza aliyestaafu upolisi huko! Kampuni moja ya Uingereza imepewa mkataba wa kushughulikia ukusanyaji kodi msumbiji!!

Kitakachofuata sasa inavyoonekana kitakuwa kutoa 'tenda' kwa makampuni ya nje kutawala nchi nzima! Ukoloni kwa 'staili' ya karne ya 21. Natoa ushahidi:

Mwaka jana mwandishi mmoja Bw. Norman Stone wa gazeti la 'The Observer' alishauri ukoloni urudi Afrika. Alisema siyo lazima ukoloni uwe kitu kibaya. Alishauri ukoloni mpya uwe wa kimsaada msaada ilimradi tu kodi iwe inapelekwa Ulaya na wao watapanga jinsi ya kutugawia tena!!! Eti kuwa viongozi wa kibongo hawatakuwa na nafasi ya 'kutia ndani' hiyo kodi itakayo kusanywa.

Mwingine naye, Bw. Robert Wheelen wa 'Institute of Economic Affairs' akaja na wazo lingine: Kwa nini tusibinafsishe bara lote la Afrika? "Makampuni yanaweza kupewa mikataba ya kutawala hizi nchi kwa kila baada ya miaka 21", alisema.

Je, sisi waafrika tuatakubali??? Usishangae tukikubali kutawaliwa tena. Nimetoa mifano hapo juu ya Msumbiji na Sierra Leone. Sasa kwa taarifa yako Libera nao wameanza kulilia kutawaliwa. Wanataka Umoja wa Mataifa ipewe nchi yao. Hata mwanasoka George Weah aliiambia gazeti la 'New York Times' kuwa Umoja wa Mataifa ingefaa iichukue Liberia na siyo kwa muda, bali moja kwa moja!

Wengine wamekuja na mawazo mengine ya ajabu zaidi. Wanasema madikteta wa Afrika walipwe pesa ili kuachia uongozi. Wanadai kuwa Somalia imeharibika na kupoteza njia kuu za uchumia zaidi ya dola bilioni 3. Kama ingetumika dola milioni 50 kununua akina Siad Barre Somalia isingekuwa kama ilivyo. Wengine wameshauri nchi za magharibi ziwe na mfuko wa kununua madikteta.

Porojo Page -HOME