Vipi biashara ya matunda?

Naona aibu sana. Aibu yangu inatokana na ukweli wa kuwa biashara ya matunda Tanzania inazidi kudidimia mwaka hadi mwaka. Maelfu ya tani za matunda yanaoza kila msimu katika kila kona ya nchi yetu.

Halafu eti tunaambiwa kuwa Che Nkapa ana dhumuni la kuboresha kilimo nchini! Kama huku ndiyo kuboresha kwenyewe, basi tuna shida.

Mtu unahitaji kutembelea mkoa wa Tanga tu ili ujionee jinsi gani kiasi cha maembe, machungwa, mapeasi, machenza, matunda damu na ndimu yanaoza tu. Kinachosikitisha zaidi ni kuwa wakulima wanaendelea kuwa maskini na kuvaa marapurapu utafikiri mitumba ya bei poa hakuna.

Mkoani Morogoro, Tabora, Pwani, Mbeya na kwengineko, matunda pia huoza tu. Hakuna wanunuzi. Tabora maembe huoza na wakazi wa mkoa huo hawawezi kuhesabu maembe kama zao la biashara. Mkoani Morogoro kuna utajiri wa mananasi machenza, machungwa na matunda damu.

Cha ajabu ni kuwa serikali yetu inajua kuwa dunia nzima iko tayaru kununua matunda yetu. Tatizo ni kuwa wanunuzi wa nje wanataka mazao yawe kwenye hali ya ubora. Nikumbusheni lakini kwani kazi ya Shirika la Viwango (TBS) ni nini? Kuweka viwango vya kondom tu? La hasha, hata viwango vya mazao ya shambani pia. Yaani ufungaji, uchaguzi na kadhalika. TBS inaweza kusaidia wakulima katika kuwaelimisha kuhusu hili.

Kinachoumiza zaidi, ni kuwa maembe ya makopo yanayotoka Dubai na kujazwa kwenye maduka ya Dar es Salaam, yamechumwa Tanzania!!! Yaani Dubai wananunua toka kwetu halafu wanatuuzia sisi tena. Aibu gani hii???

Kingine ni kuwa matunda yanahitajika sana nchi ya jirani Kenya. Lakini watanzania tumeshindwa kuwauzia hata ndugu zetu wa jirani. Hata vitunguu vyetu wanavitaka, lakini hakuna wa kuwapelekea!

Sisi watanzania tuliichagua hii serikali ituongoze katika maswala kama haya. Serikali kazi yake ni kutusaidia ili tujisaidie. Sasa Che Nkapa anasema eti watanzania wavivu. Uvivu gani huo wa kulima mashamba ya mananasi na vitunguu lakini kukosa wanunuzi? Yaani inakuwaje watu milioni 30 walioko Tanzania leo hii wanashindwa kumaliza matunda mpaka yanaoza? Wakenya wapo tayari kununua lakini hakuna wa kuwapelekea?

Viwanda vya kutayarisha matunda viko wapi? Au tuwalete na waafrika kusini au wamarekani nao watusaidie kujenga viwanda vya kusindika matunda?

Lakini kuna vitu fulani watu kama sisi tunaelewa kinachoendelea. Kodi kubwa ya kuingiza mashine na ukiritimba wa hali ya juu ni mojawapo ya vikwazo.

Che Nkapa umebakiza miaka minne tu. Kazi kwako.

Porojo -HOME